Sifa njema zote ni za Mwenyezi Mungu, Mola wa tawfiki na uongofu, Mwenye kumfikisha mkweli katika kumwelekea yeye hadi kufikia upeo wa mwisho. Tunashuhudia kwamba hapana Mola apasaye kuabudiwa kwa haki isipokuwa Mwenyezi Mungu pekee, hana mshirika; Kwake yeye ni marejeo ya mambo yote, mwanzo na mwisho. Na tunashuhudia kwamba bwana wetu na Mtume wetu Muhammad ni mja wake na Mtume wake, mwenye upeo wa mwisho katika uzuri wa kufikisha ujumbe kutoka kwa Mwenyezi Mungu na kuwaongoza watu kwa Mwenyezi mungu Mtukufu katika utukufu wake; Mbora wa aliepokea maneno ya Mola na akatekeleza amana kwa ajili ya kutengamaa katika siri na dhahiri.
Ewe Mwenyezi Mungu, mshushie Rehema, Amani na Umbariki mja wako mteule, Mtume wetu Muhammad, na Ahli zake waliotakaswa na uchafu, na Maswahaba wake wenye nyuso zenye kung’ara; waliopokea kwake ujumbe kutoka kwako na wakautekeleza kwa utekelezaji bora; na kwa wale walio watawalia nakuwapenda kwa ajili yako na wakawa na msimamo katika njia yao; na juu ya baba zake na ndugu zake miongoni mwa Manabii na Mitume wako watukufu; na juu ya Ahli zao na Maswahaba zao na watu wa kuigwa na kufuatwa; na juu ya Malaika wako waliokaribu na watukufu; na juu ya waja wako wote walio wema; na juu yetu pamoja nao na miongoni mwao kwa rehema zako, Ewe Mwenye utukufu na heshima.
Ama baad:
Kwa ndugu zetu wote kwa ajili ya Allah Tunaleta wasia wa kuitukuza Dini ya Mwenyezi Mungu na kuitumikia Sharia ya Mwenyezi Mungu – Aliyetukuka Utukufu wake na Aliyetukuka katika Ukubwa wake. Na miongoni mwa misingi ya juu kabisa katika kuitumikia Sharia ni kupokea elimu ya sheria iliyo lindwa mapokezi yake, kwa ajili ya kuifanyia kazi, kuifundisha na kuieneza sehemu mbali mbali. Na msingi huo unajumuisha kila kinachotokana na ukweli na uzuri wa kutumikia katika kumnusuru Mwenyezi Mungu na Mtume wake Rehema na Amani zimshukie Mtume, Ahli zake na Maswahaba zake.
Na ikawa miongoni mwa mchango katika uwanja huu na jambo hili ni kuanzisha Chuo cha Sanad kwa ajili ya kuifikia elimu na kwa ajili ya kuifanyia kazi na kujitakasa, na kwa ajili ya kulingania kwa Mwenyezi Mungu Mtukufu. Kwa hakika hadhi ya elimu na utukufu na Daraja lake, Kuipuuza elimu na kuidharau kwake kumesababisha matatizo na maharibiko mengi katika maisha ya watu. Kisha kuichukua elimu kwa njia isiyo sahihi na sehemu isio sahihi, na kwa watu wasio sahihi, na kwa mwenendo usiokua wa Maswahaba, Tabiina na waliowafuata kwa wema—hilo pia limesababisha matatizo ambayo wakati mwingine huwa makubwa na mazito kuliko matatizo ya kuipuuzia au yale yaliyosababishwa na kuipuuzia elimu katika matatizo na maharibiko ya umma.
Na kuhusiana na hilo, amesema bwana wetu Umar bin Al-Khattab radhi za Mwenyezi Mungu ziwe juu yake “Hofu kubwa ninayo ikhofia zaidi katika umma ni munafiki mwenye elimu.” Wakasema: “Vipi awe munafiki ni mwenye elimu?” Akasema: “Mjuzi wa kuzungumza, Mjuzi wa kuzungumaza.. lakini moyoni mwake ni munafiki.”
Na hivyo ndivyo madhara yanavyopatikana katika kuchukua elimu kutoka kwa wasio watu wake na bila ya mapokezi sahihi. Lakini kwa kuungana na kuitukuza elimu ya sheria na kuikuza na kuiheshimu na kuichukua kutoka kwa watu wake na wahusika wake, na kutekeleza na kupitisha hukumu zake na kuzifanyia kazi na kuieneza elimu kwa viumbe—hupatikana kwa hilo kuziba kila pengo, kuondoa kila upotovu na makosa, na kuondosha kila kilichotatanisha na kilichozidi kuwa kigumu miongoni mwa matatizo na maradhi.
Kwa sababu hiyo tunamsifu Mwenyezi Mungu aliyerahisisha sababu hizi za kuungana na Chuo cha Sanad. Hakika katika zama za Maswahaba na waliokuja baada yao walikua wakisafiri mwendo wa miezi miwili kwa ajili ya kuchukua hadithi moja kwa Mapokezi sahihi, kwa sababu walitambua utukufu wa elimu, utukufu wa hadithi na utukufu wa mapokezi sahihi hadi kwa Mtume – Rehema na Amani ziwe juu yake. Na Mwenyezi Mungu amerahisisha sasa vifaa na njia hizi za kupokea elimu hii, kuifafanua na kuipanga kulingana na mtaala uliowekwa katika Chuo cha Daru Al-Mustafa, na kupanda daraja katika malezi ya kielimu katika kufundisha elimu ndogo kabla ya elimu kubwa, na kwa kuendelea kwa utaratibu hadi kupanuka kwa mtindo uliopokelewa kutoka kwa watu wakweli, na wenye elimu nyingi na ujuzi mkubwa – radhi za Mwenyezi Mungu mtukufu ziwe juu yao. Mwenyezi Mungu akarahisisha kuzinduliwa Program hii katika Chuo hiki: na katika muda mchake wa majaribio wamejiunga na Chuo hiki idadi inayozidi elfu nane, takriban elfu nane na mia sita (8600).
Basi Program hii ni Sababu, Chombo na Uwanja wa kuitumikia Sharia na Dini, na kuungana kwa kina na huduma hii kwa upande wa kufundisha na kupokea elimu kutoka kwa wenye mapokezi sahihi na muunganiko na Wanawazuoni wa Dini hii na Sharia tukufu, kutoka kwa kila mkweli mwenye heshima – “Hizi ni fadhila za Mwenyezi Mungu humpa amtakaye.” Natunapenda kuwa na juhudi ya kukuza sehemu hii ya faida hizi ili yapatikane matunda mazuri kwa umma huu kwa kheri ambazo zitakunjua uwanja kutokana na siri ya mafungamano ya nyoyo katika elimu, ladha, vitendo na mafundisho kutoka kwa Mtume – Rehema na Amani ziwe juu yake – na wahyi alioletewa na Mwenyezi Mungu na yote aliyoteremshwa juu yake.
Mwenyezi Mungu azifungue nyoyo, na awabariki wote wanaosimamia kheri hizi na wote wanaochangia na kusaidia katika kueneza sababu hizi zenye nguvu za kuhuisha njia iliyo sawa katika kupokea elimu za kisheria kwa ajili ya kuzifanyia kazi, kuzifundisha na kuzieneza kwa kutafuta radhi za Mjuzi wa yaliyo wazi na yaliyo fichikana, Mola wa viumbe. Mwenyezi Mungu awape taufiq, awaongoze, na awape furaha wote waliokuja na walio somesha na walio soma katika sehemu hii; Na awajaalie wawe katika msaada wake na uangalizi wake na uangalizi wa Kipenzi chake Mwaminifu – Rehema na Amani ziwe juu yake – na atukusanye kwao katika daraja za juu pamoja na wema wa viumbe, kwa upole na uzima. Mwenyezi Mungu aiboreshe hali ya umma na awaondolee kila huzuni, awafungulie njia na awape taufiki ya kusimama imara katika njia hiyo iliyonyooka na tukufu, kwa upole na uzima. Hakika yeye ndiye Mkarimu wa wakarimu, kwa siri ya Surat Al-Fatiha hadi kwa Mtume Muhammad – Rehema na Amani ziwe juu yake.